Tanzania

Tanzania ina idadi kubwa ya simba barani Afrika, ikiwa na takribani ya asilimia 40 ya idadi ya simba duniani, pia ni ya tatu kwa idadi kubwa ya tembo barani Afrika. Ina mbuga 22 za kitaifa, na asilimia 39 ya ardhi yake inalindwa rasmi kwa ajili ya wanyamapori. Lakini wanyamapori wengi Tanzania bado wanatumia sehemu ya muda wao mwingi nje au kuzurura kati ya mbuga za wanyama. Kwa kiasi fulani, wanyamapori nchini Tanzania wanakabiliwa na vitisho vingi, vikiwemo migogoro na binadamu, uwindaji wa nyama pori, ujangili, upotevu wa makazi na mabadiliko ya tabia nchi. 

Kwa mustakabali wa uhifadhi, ni muhimu kutafuta njia kwa wanadamu na wanyamapori kuishi pamoja. Tunaamini Tanzania inaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa Afrika nzima. Pia tunaelewa kuwa jamii zinazopata pesa kutokana na kuwahifadhi wanyamapori wana uwezekano mkubwa wa kuwalinda na kuwahifadhi, na hivyo kusababisha kupungua kwa ujangiri, uwindaji haramu, na mauaji ya kulipiza kisasi.

WildAid imejitolea kusaidia maeneo ya hifadhi za jamii (WMAs) nchini Tanzania, kwa kushirikiana na Honeyguide Foundation na Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (CWMAC). Hifadhi jamii zimeanzishwa ili kulinda wanyamapori na makazi yao kwenye njia kuu za uhamiaji na maeneo ya mtawanyiko nje ya hifadhi, huku zikitoa fursa za kiuchumi kwa jamii kupitia biashara zinazoletwa wanyamapori. Muungano huo unalenga kuanzisha hifadhi jamii 12 zinazojiendesha kiuchumi, huku mapato yatokanayo na utalii na biashara ya hewa ukaa (carbon credits) yakifadhili shughuli zao na kuhamasisha jamii kuhifadhi rasilimali za wanyamapori.

Ili kuhakikisha mafanikio ya hifadhi jamii, tunaamini katika kuwezesha jamii na kuwapatia zana wanazohitaji ili kulinda na kufaidika na wanyamapori. Hii ni pamoja na kutoa mafunzo kwa viongozi wa jumuiya kuhusu mikakati madhubuti ya mawasiliano, kusaidia uundaji wa mipango ya muda mrefu ya kuvutia wawekezaji katika utalii na mapato ya biashara ya hewa ukaa, na ushawishi katika ngazi ya wilaya na kitaifa ili kusaidia sera zinazowezesha uendelevu wa kifedha katika hifadhi jamii. 

Mtazamo wetu pia unajumuisha kuwezesha vyombo vya habari kwa kutoa maudhui ya uhifadhi na mafunzo kwa waandishi wa habari kutoa ripoti za mara kwa mara kuhusu manufaa ya wanyamapori, kubadilisha mtazamo kutoka kwenye migogoro ya binadamu na wanyamapori hadi kutegemeana kati ya binadamu na wanyamapori, na kuleta mabadiliko ya kweli na ya msingi.

 

Takwimu muhimu

•    Tanzania ni ya tatu kwa idadi kubwa ya tembo barani Afrika.

•    Tanzania ilipoteza asilimia 60 ya tembo wake ndani ya miaka mitano hadi kufikia mwaka 2014, lakini sasa idadi ya tembo immeongezeka kwa kiasi fulani.

•    Ujangili umepungua kwa asilimia 70 kutoka viwango vya juu.

•    Mwaka 2019, utalii ulichangia asilimia 10.7 ya pato la taifa na kuajiri zaidi ya watu milioni 2.

•    Mwaka 2019 Tanzania ilipata dola bilioni 2.6 sawa na shilingi trilioni 6 kutokana na utalii, kiasi ambacho kilitokana na watu wa nje na ndani waliotembelea hifadhi za taifa kujionea wanyamapori.

•    Kuna takribani simba 20,000 tu hivi sasa barani Afrika. Karne moja iliyopita, kulikuwa na simba 200,000 barani Afrika. Kupungua huku kumetokea kwa wingi katika miongo miwili iliyopita.

•    Simba walikuwa wakipatikana sehemu nyingi za Afrika; leo hii wametoweka kwa  asilimia 94 katika ukanda huo.

•    Takribani 40% ya simba wa Afrika wako Tanzania, wengi wao wanaishi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Idadi ya simba inapungua hata Tanzania.

•    Hii inatokana zaidi na ukweli kwamba asilimia 60 ya simba wa Tanzania wanaishi nje ya maeneo ya hifadhi, jambo ambalo linawafanya kukabiliwa na vitisho vingi.

 

 

#bethepride

Mwaka 2019 WildAid ilizindua kampeni ya “be the pride” nchini Tanzania, ikionyesha thamani ya kuwalinda simba kwa taifa na dunia. Kupitia televisheni, mabango, mitandao ya kijamii, na redio, tumesambaza ujumbe kutoka kwa watu mashuhuri, wanasiasa na mashujaa wa uhifadhi wa ndani kuhimiza hatua za pamoja kuwalinda simba na makazi yao. Kampeni inaangazia umuhimu wa simba kwa uchumi, kwa urithi wa Afrika na kwa mazingira.

 #Jointheherd

Mwaka 2015, WildAid ilianzisha kampeni ya “Join the herd” nchini Tanzania yenye kauli mbiu “Ujangili unatuibia sote”. Kwa kuungwa mkono na watu mashuhuri, kampeni hiyo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuongeza ufahamu juu ya masaibu ya tembo na umuhimu wa kuwalinda. Kwa ushirikiano na baraza la viongozi wa dini la Tanzania tulichapisha kitabu kinachoonyesha jinsi mafundisho ya kidini yanavyosaidia ulinzi wa wanyamapori. Tangu wakati huo, serikali ya Tanzania imeimarisha utekelezaji wa sheria kuhusu uhalifu wa wanyamapori, na hivyo kupelekea mfanyabiashara mchina aliyejulikana kwa jina la utani la malkia wa pembe za ndovu kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela mwaka 2019 kwa kuendesha mojawapo ya mitandao mikubwa ya biashara za magendo barani Afrika uliopo nje ya Tanzania. Idadi ya tembo nchini Tanzania imeongezeka hadi 60,000 mwaka 2019 kutoka 43,000 mwaka 2014.

Faida za kuongezeka kwa idadi ya simba

  • Utalii na Uchumi - Simba ni moja ya wanyama watano wakubwa mashuhuri “the big five”, na ya juu katika orodha ya wanyama ambao watalii huja Tanzania kuwaona. Wanyamapori ndio kichocheo kikuu cha utalii nchini Tanzania na hutoa mamilioni ya ajira kuanzia sekta ya utalii na ukarimu, usafirishaji hadi miundombinu. Mapato yanayopatikana kutokana na utalii yanasaidia maendeleo ya nchi kwa kutoa fedha za kuboresha huduma muhimu kama vile shule, barabara, hospitali na upatikanaji wa maji.
  • Uwiano wa Mazingira - Simba wanajulikana kama spishi zinazoleta uwiano katika mfumo wa ikolojia, kuishi kwa wanyama wengine kunategemea wao. Simba hudhibiti idadi ya wanyama wanaokula majani, kuzuia malisho kupita kiasi na uharibifu wa ardhi. Hii inahakikisha kwamba udongo unabaki imara na wenye rutuba, vyanzo vya maji havikauki na hali ya hewa inadhibitiwa. Simba pia huua mawindo dhaifu au wagonjwa kuzuia magonjwa kuenea kwa mifugo yetu. Yanapohifadhiwa, makazi ya simba pia ni "mizizi ya kaboni" (carbon sinks) ambayo uhifadhi hewa ya kaboni ambayo ingeweza kuenea angani na kuchochea mabadiliko ya tabia nchi. Hii inaathiri kila kitu kuanzia upatikanajii wa maji hadi mazao tunayopanda. Tazama video hii kwa habari zaidi:
  • Urithi, Utamaduni na Utambulisho - Simba ni ishara ambayo makabila mengi nchini Tanzania hujumuisha katika hadithi, sanaa na ngoma. Chapa na mashirika mengi nchini pia yanajitambulisha kwa alama ya simba kwa sababu ya kile wanachowakilisha - sifa kama vile nguvu, ukuu, uwezo na uthabiti. Simba wapo kila mahali kuanzia noti zetu za shilingi hadi majina ya vilabu vya soka, na hadi mifuko ya saruji, pakiti za viungo na biskuti.