WildAid imezindua filamu ya Tanzania: Taifa la Simba/Tanzania: Land of the Lion, inayoonyesha nafasi ya Watanzania katika kuhifadhi idadi kubwa ya simba duniani. Tulizungumza na mtaalamu wa dawa za asili za Kimasai, Noah Salonick, kuhusu utamaduni wa Wamasai na jinsi unavyosaidia kuhifadhi mazingira asilia.
Wakati Noah Salonick alipokuwa akikua, aliwaheshimu sana babu zake. Katika jamii ya Wamasai, waliheshimiwa sana, kama wataalamu wa dawa za mitishamba walikuwa "tajiri na maarufu". Hivi sasa akiwa na umri wa miaka 42, anajivunia kufuata nyayo zao, akifanya kazi kama mtaalamu wa mitishamba kwa miaka 17 iliyopita.
Amezunguka nchi mbali mbali kama vile Sudan Kusini, Kenya na hata Msumbiji akipeleka dawa za asili za Kimasai kwa watu wa Afrika. Lakini pia huzunguka katika ardhi ya Wamasai pia, akitafuta viungo sahihi.
"Dawa hazitengenezwi kwa kitu kimoja au mti mmoja au miwili pekee - baadhi ya mitishamba inahitaji majani, wakati mingine inahitaji mizizi au aina maalum za miti," alisema. “Unakusanya mitishamba mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali hadi upate kila kitu unachohitaji. Kwa mfano, mimea aina moja inaweza kupatikana katika mlima fulani, na mimea mingine inaweza kupatikana katika mlima tofauti.”
Kama vile ilivyo kuishi pamoja na simba kunavyoingiliana sana na mila ya Wamasai, ndivyo hivyo pia hata kwa dawa za mitishamba, anasema. Vyote viwili vinachangia katika urithi mkubwa wa tamaduni za kitanzania.
Pia kuna uhitaji mkubwa wa dawa za kimasai, anasema.
"Madawa ya asili ya Wamasai yanazidi kuwa maarufu kwa sababu yanafaa - kizuri chajiuza," alisema. "Dawa za Magharibi zinaweza kukuhitaji kumeza vidonge viwili mara tatu kwa siku, lakini kwa dawa zetu, hata ukinywa lita moja, haina madhara yoyote."
Licha ya umaarufu wa tiba za mitishamba, Salonick ana wasiwasi kuhusu siku zijazo. Ni vijana wachache sana, anasema, wanaotamani kuwa wataalam wa dawa za kienyeji au kurithi fani hiyo kutoka kwa babu zao.
"Ni tofauti na kizazi chetu," alisema. “Watoto wanaona mtu bungeni na kusema, ‘Ninataka kuwa kama mtu huyo, si kama babu na bibi yangu.’
Shinikizo la mazingira linasababisha uhaba mwingine.
"Upatikanaji wa dawa umekuwa changamoto, hasa kwa sisi Wamasai," alisema. "Kwa karibia asilimia 70 kutokana na ukataji miti kwa ajili ya mbao na mkaa."
"Tanzania: Taifa la Simba" inaonyesha faida za uhifadhi wa kijamii
Salonick aliiomba serikali ya Tanzania kujitahidi zaidi kulinda misitu na mimea inayoota huko.
"Serikali inamiliki misitu, na inadhibiti misitu," alisema. “Kwa upande wa jamii yetu hatukati miti wala kutumia mkaa, bali miti inapungua kutokana na watu kuikata kwa manufaa yao binafsi."
Wakati kuna ofisi ya dawa za asili katika kila mkoa wa Tanzania, Salonick analalamika kwamba watu wanaofanya kazi huko sio wenyeji ambao ni wataalam wa dawa za asili, na sio dawa zote ni halisi.
"Ni kama bidhaa ghushi. Baadhi ya watu wanaziuza bila kuwa na ujuzi wala uzoefu wa tiba asilia,” alisema.” Watu wanaoishi mijini wameanza kutuharibia kazi kwa sababu ukimwambia mtu dawa hii inatibu hali fulani na mtu huyo hapati nafuu. , wataelewaje?
Licha ya wasiwasi huu, Salonick anasema anajivunia kazi yake, na utajiri wa ujuzi unaotokana na kazi hiyo.
"Labda katika siku za usoni, watu watatambua kuwa Wamasai wanauza bidhaa halisi, na unaposema wewe ni mtaalam wa tiba asilia ya Kimasai, watajua unachomaanisha."