Katika maeneo mbali mbali Tanzania, daima Simba amekuwa alama ya nguvu na fahari ya Kiafrika, wakiashiria nguvu, ujasiri, na umoja. Hata hivyo, idadi ya simba duniani kote imepungua kutoka 200,000 karne iliyopita hadi karibu 20,000 hivi leo, hasa kutokana na upotevu wa makazi yao kutokana na shughuli za binadamu. Tanzania ni mojawapo ya ngome za mwisho za simba, ikiwa na idadi kubwa ya simba duniani. Ikikadiriwa kuwa na takriban simba 8,000. Mafanikio haya makubwa ya uhifadhi yanatokana na juhudi kubwa za serikali na watanzania wengi kuhakikisha simba wanafanikiwa pamoja na nchi na watu wake.
Filamu mpya iliyotolewa na WildAid pamoja na washirika wake, inayoitwa Taifa La Simba, inaangazia mafanikio makubwa yaliyofikiwa na watanzania katika kulinda viumbe hawa wa kipekee, pamoja na jukumu muhimu la jamii katika kuhifadhi uwiano kati ya binadamu na wanyamapori. Ni hadithi inayotia tumaini na kukumbushia faida zinatotokana na maliasili, na umuhimu wa wanyamapori kwa mustakabali endelevu kwa ajili yetu sote.
Simba ni muhimu kwa utalii nchini Tanzania. Utalii wa wanyamapori unachangia karibu 17% ya pato la taifa la Tanzania na kutoa ajira zipatazo milioni 1.5, huku simba wakiwa kivutio kikubwa. Simba mmoja anayeishi kwa miaka 10 anaingiza takriban shilingi za kitanzania bilioni nane (dola milioni 3) katika mapato ya utalii. "Wageni wengi wavyokuja kutembelea nchini yetu kwa ajili ya kufanya utalii, wanapendelea kumuona simba," alisema Alfred Sakita, ambaye amekuwa akifanya kazi ya kuongoza watalii kwa miaka 21. "Kwa kuwa simba ni mnyama mmoja hodari. Ni mnyama ambaye anayejulikana kama mfalme wa mbuga au mfalme wa pori."
Simba pia hutoa manufaa mengine muhimu kwa jamii zinazoishi kando yao, na kutoa mapato ambayo huboresha upatikanaji wa elimu, huduma za afya, na huduma za matibabu ya mifugo. "Kutokana na uwepo wa wanyamapori… nasi kama kituo tumeweza kutoa huduma kwa wakati, nakuweza kuwa na vifaa tiba vya kutosha, pamoja na dawa", alisema ofisa wa kliniki wa kituo cha afya cha makifu, kinachopakana na hifadhi ya taifa ya Ruaha. Maili kumi na mbili (km 20) kaskazini, Abdallah Rashid, mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Kitisi, alionyesha athari chanya ya msaada wa jamii unaotolewa na mashirika ya uhifadhi. "Kupitia chakula watoto wanapata mahudhurio mazuri," alisema. "Kupitia madawati pia, tulikuwa na uhaba, watoto walikua wanakaa zaidi ya watatu hadi wanne. Kwa hiyo sasa hivi watoto wanakaa wawili wawili kwenye madawati."
Umuhimu wa simba kwa Tanzania ni zaidi ya faida za kiuchumi wanazoleta. Utamaduni wa kimaasai umekuwa ukiwaheshimu sana simba. Hata hivyo, ingawa wamaasai walikuwa wakiamini kwamba kijana anapaswa kumuua simba ili awe shujaa, wao wamebadili tamaduni zao ili kuishi na simba. Wamasai sasa wanasherehekea mila na desturi zao bila kuwadhuru simba, bali kwa kuwalinda. "Zamani tulikuwa tunaua simba, na tulikuwa tunawaona kama adui," alisema mwanajamii wa kimasai, "tunafahamu kwamba hawa simba ni mmoja wa wanyama ambao ni muhimu sana duniani, sio hapa tu kwetu. Kwahiyo tukiwa moja wa jamii ambayo wanaweza kuhifadhi hawa wanyama; Inatupa nguvu na pia inatupa hamu ya kuwa moja ya watu wanaohifadhi wanyama hawa”.
Uhifadhi wa simba na makazi mengine ya wanyamapori nchini Tanzania pia hutoa manufaa ya kimazingira, kama vile upatikanaji wa maji safi kwa shughuli za binadamu na mifugo. Misitu, mito, na nyasi ni muhimu kwa maisha ya simba, lakini pia ni muhimu kwa maisha ya watu. Kulinda makazi haya kunahakikisha kuwa watu wanapata maji kwa shughuli za kibinadamu na mifugo. Mazao kama vile nyanya yanaweza kustawi kutokana na upatikanaji wa maji yanayotolewa na mito katika mazingira haya, na kuuzwa katika miji, kutoa chakula kwa watu na maisha ya kiuchumi kwa wakulima.
Watanzania wanaungana ili kulinda urithi wao wa kipekee wa wanyamapori na kutafuta mustakabali mwema kwa simba na jamii za wenyeji. Wakati sehemu nyingine za dunia zimehatarisha maisha ya wanyamapori wao katika kutafuta maendeleo ya kiuchumi, Tanzania ina fursa ya kuonyesha mtazamo bora zaidi.
Changamoto iko katika kuhifadhi urithi wa kitamaduni na asili wa taifa kwa namna ambayo inaruhusu watu na wanyamapori kustawi kwa pamoja. Kwa kuwa msitari wa mbele kimataifa katika uhifadhi wa simba, watanzania wanaweza kuendeleza sifa ya nchi yao kama Taifa la Simba na kuhamasisha ulimwengu kuiga mfano huo.
Tazama filamu na ujifunze zaidi kuhusu jukumu muhimu la jamii za wenyeji katika juhudi za uhifadhi wa simba nchini Tanzania.